Rais Kikwete achoshwa na vurugu za wapinzani....Awataka wanaCCM kuacha unyonge na badala yake wajibu mapigo ya vurugu hizo, asema uvumilivu una ukomo wake
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewataka wanachama wake kuacha
unyonge na kujibu mapigo ya wapinzani hasa wale ambao wanaendesha siasa
za vurugu katika kampeni za chaguzi mbalimbali nchini.
Rais
Kikwete amesema kuwa uvumilivu una ukomo, na kwamba sasa wanachama wa
CCM hawana budi kuacha unyonge, kutokana na siasa hizo za vurugu
zinazoendeshwa na vyama vya upinzani.
Aliyasema
hayo jana mjini Dodoma wakati akifungua kikao cha kawaida cha
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kitakachokutana kwa siku mbili
chini ya uenyekiti wake, ambacho ajenda kuu ni kuzungumzia Bunge Maalumu
la Katiba.
“Tumelizungumzia hili katika Kamati Kuu, tumekubaliana kuacha unyonge (makofi). Ndiyowatu wamelisema hili katika Kamati Kuu, tumesema jamani tumekubaliana kuacha unyonge,”
“Wacha wakaseme (waandishi wa habari), ndio tumekubaliana kuacha unyonge. Kabisa. Hata kama leo katika taarifa za habari, zisiwekwe habari nyingine, msikike ninyi tu. Uvumilivu una ukomo wake.”
alisema Rais Kikwete ambaye wakati anafungua kikao hicho waandishi wa habari walikuwamo.
Mwenyekiti
huyo wa CCM alisema wamefikia hatua hiyo kwa sababu yanayotokea
yanasikitisha sana na akatoa mfano wa matukio kadhaa ya uvunjifu wa
amani katika kampeni katika maeneo ya Igunga mkoani Tabora na Kahama
mkoani Shinyanga.
“Maana tunashindana na wenzetu wagomvi maana wao ugomvi ndio sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya siasa. Maana pale Kahama kijana wamemtoa macho kwa bisibisi. Acheni unyonge (makofi).
“Nasema kwa kweli kwa sababu yanayotokea yanasikitisha. Pale Igunga kijana yule wamemmwagia tindikali, pale Kahama kijana wamemtoa macho kwa bisibisi. Tuache unyonge,”
alisisitiza Rais Kikwete huku akishinikizwa kwa shangwe za CCM Oyee, Mapinduzi Daima.
Ingawa
Rais Kikwete hakutaja chama, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimekuwa kikihusishwa na vurugu za uchaguzi katika maeneo
mbalimbali yakiwamo ya Igunga na Kahama katika uchaguzi mdogo wa
madiwani uliofanyika hivi karibuni na pia katika chaguzi ndogo za
ubunge.
Akizungumzia
uchaguzi mdogo wa kata 27 zilizofanyika hivi karibuni na CCM kuzoa kata
23, Rais Kikwete aliwapongeza wanaCCM kwa ushindi huo, lakini akawapa
changamoto ya kuhakikisha wanarejesha kata hizo nne zilizokwenda kwa
vyama vya upinzani.
“Huu ni ushindi mkubwa sana, ushindi mnono. Ni vizuri kutumia nafasi hii kujipongeza na kuwapongeza wenzetu kwa kazi nzuri, kazi nzuri waliyoifanya ya kujenga chama,”
“Lakini tukumbushane kwamba kata nne hatukuzipata, hivyo tuna kazi ya kuzikomboa, sisi wakati wote nia yetu ni kushinda, kushindwa haiwezekani.”
alisema Mwenyekiti huyo wa CCM na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Aidha,
alizungumzia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, akisema
hadi sasa hali ni shwari, hakuna migawanyiko wala misukosuko kama
ilivyokuwa kwa Jimbo la Arumeru Mashariki ambalo alisema tangu mwanzo
hadi mwisho, hali haikuwa shwari.
Alisema
hadi sasa wana uhakika wa ushindi katika jimbo hilo, lakini akawataka
wanaCCM kujiandaa vyema kwa kila hali na kuhakikisha ushindi unapatikana
katika jimbo lililoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri wa
Fedha, Dk William Mgimwa. Mwanawe Geoffrey ndiye mgombea wa CCM.
Pia
aliwataka wanachama na viongozi wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, nao
kujiandaa kwa uchaguzi mdogo kwa sababu tayari Spika wa Bunge, ametoa
taarifa serikalini kuhusu kuwa wazi kwa jimbo hilo kutokana na kifo cha
mbunge wake, Said Bwanamdogo.
“Msikae tu kusubiri na kuendelea kuomboleza, kwa sababu Serikali haiombolezi, wao wanachotaka ni uchaguzi ujazwe, shughuli ziendelee. Maana watu wanaweza kusema hata orobaini bado. Kule Arumeru tuliambiwa tumbo bado halijapasuka. Kwani kwa Mgimwa orobaini tayari, mbona mchakato umeanza.
“Ninyi fanyeni mchakato, orobaini yetu mnaweza kufanya wakati mambo mengine yakiendelea. Tujiandae mapema ili kuhakikisha tunashinda,”
alisema
Mwenyekiti huyo wa CCM na kuwapongeza viongozi wa mkoa na wilaya
waliofanikisha ushindi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki
ambako mgombea wao, Mahmoud Thabit Kombo alishinda.
Alisema
CCM ilibidi kumtosa aliyekuwa mbunge wao, Mansour Yussuf Himid, kwa
sababu alikuwa akivaa magwanda ya chama hicho, lakini alikuwa akipinga
sera na taratibu za chama hicho tawala.
“Kila akifungua mdomo wake anaitukana CCM, kila akifungua mdomo anapingana na sera za CCM. Tukasema inatosha, bora kuwa na mpinzani huko nje kuliko huyu, ndio maana niliwahi kusema katika NEC moja hapa kuwa sijui mtu anasema nitahama CCM, nikasema nendeni sasa hivi,”
alisema Kikwete.
No comments:
Post a Comment